Wananchi Bunda wapewa somo kuepuka athari za kiboko
28 April 2024, 3:02 pm
Kufuatia matukio yaliyoripotiwa wiki iliyopita ya kiboko kujeruhi na kuua, Afisa Wanyamapori TAWA atoa somo namna ya kuepuka athari za mnyama huyo
Na Edward Lucas
Wananchi wameaswa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Kiboko na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika pindi wanapogundua uwepo wa mnyama huyo katika makazi ya watu ili kuepusha madhara kwa mali na maisha ya watu.
Wito huo umetolewa na Afisa Wanyamapori kitengo cha Ujirani Mwema TAWA Kanda ya Ziwa, Lusato Masinde kupitia Radio Mazingira Fm kipindi cha Uhifadhi na Utalii akitoa elimu zaidi kuhusu mnyama Kiboko na tahadhari wanazotakiwa kuchukua wananchi ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mnyama huyo.
Lusato amesema Kiboko ni miongoni mwa wanyama wakubwa na hatari zaidi wanapokuwa karibu na binadamu hivyo amewataka wananchi kujiepusha kufanya shughuli zao maeneo wanapopatikana wanyama hao na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika pindi watakapomuona anaingia katika makazi ya watu ili adhibitiwe mapema asilete madhara kwa mali na maisha ya watu.
Kufuatia matukio yaliyoripotiwa hivi karibuni ya watu kushambuliwa na mnyama Kiboko ikiwa ni pamoja na tukio la Juma Ryoba Waise maarufu Kebuchwa(55)mkazi wa Kijiji cha Mihingo Wilaya ya Bunda kufariki dunia kwa kushambuliwa na mnyama huyo huku Makuru Matambari (50) mkazi wa Kitongoji cha Nyabusegesi Kijiji cha Remung’orori Wilaya ya Serengeti akinusurika kifo siku moja baada ya kifo cha Kebuchwa, Mazingira Fm imemualika Afisa Wanyamapori katika Kipindi cha Uhifadhi na Utalii ili kutoa Elimu zaidi kuhusu mnyama huyo na tahadhari zinazotakiwa kuchukuliwa ili kuzuia madhara zaidi kwa jamii.