Radi yaua mtoto Bunda, mwingine ajeruhiwa wakiwa ndani
17 April 2024, 11:55 pm
Mtoto mmoja afariki dunia na wengine watatu wanusurika kifo huku mwingine akijeruhiwa vibaya baada ya kupigwa radi wakiwa ndani ya nyumba kujikinga mvua.
Na Edward Lucas
Magreth Gomisi (7) amefariki dunia na ndugu zake watatu wakinusurika kifo huku mmoja akiwa amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na radi wakiwa ndani ya nyumba kijiji cha Kihumbu kata ya Hunyari Halmashauri wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Tukio hilo limetokea jana tarehe 15 April 2024 majira ya saa 11:00 jioni wakati watoto hao wa familia moja wakiwa ndani ya nyumba huku mvua akiwa iliyoambatana na radi ikiendelea kunyesha.
Akizungumza na Radio Mazingira Fm, jirani ambaye ni shuhuda wa tukio hilo Peter Mandazi mkazi wa kijiji cha Kihumbu amesema wakati mvua inanyesha walisikia sauti kubwa ya radi ikipiga karibu na maeneo yao na baada ya dakika chache kutoka nje ndipo walipoona nyumba ya Gomisi Mtoni ikiwa inawaka moto na kulazimika kwenda kwa haraka kutoa msaada.
Gomisi Mwesta Mtoni ambaye ni baba wa watoto hao amesema wakati tukio linatokea yeye na mke wake hawakuwepo nyumbani ambapo amewataja watoto wanne waliokuwepo kuwa ni Juma (13), Annastazia(9) ambao wote walinusurika.
Magreth (7) ambaye ni marehemu kwa sasa na Neema (11) ambaye alijeruhiwa vibaya kwenye tukio hilo na anaendelea kupata matibabu katika hospitali ya Bunda DDH.
Loyce Justine ambaye ni muuguzi wa zamu wodi ya watoto hospitali ya Bunda DDH amesema mtoto Neema anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata kwa kuungua sehemu mbalimbali za mwili wake na hali yake kwasasa ni unaendelea vizuri ikilinganishwa na kipindi anafikishwa hospitalini hapo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kihumbu, Daniel Reuben Isengese amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari hasa kwa kuangalia usalama wa watoto kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimesababisha athari mbalimbali katika kijiji hicho.