Viongozi wa kata CCM Bunda wapewa pikipiki
17 April 2024, 6:09 am
Pikipiki 132 zimetolewa kwa viongozi wa Kata 33 CCM Bunda kwa lengo la kuimarisha uhai wa chama.
Na Adelinus Banenwa
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Ndugu Mayaya Abraham Magese amekabidhi pikipiki kwa makatibu wa CCM wa chama na Jumuiya zake ngazi ya kata wilayani Bunda.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi za CCM mjini Bunda Ndugu Mayaya amesema pikipiki hizo zimetolewa na mwenyekiti wa CCM taifa Ndugu Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo kuu la kuimarisha uhai wa chama.
Mayaya amesema pikipiki hizo zimetolewa kwa makatibu hao Tanzania nzima na kwa wilaya ya Bunda wamepata pikipiki 132 kwa jumla ya kata 33 zinazounda wilaya ya Bunda.
Aidha amesema wanufaika wa pikipiki hizo ni Katibu wa CCM ngazi ya kata, katibu wa jumuiya ya wazazi ngazi ya kata, katibu jumuiya ya UWT ngazi ya kata pamoja na katibu wa jumuiya ya Vijana ngazi ya kata hivyo kufanya kila kata kupata pikipiki nne (4).
Mayaya amesema katika ziara inayoendelea ya kamati ya siasa kwenye kata moja ya changamoto kubwa ambayo wamekuwa wakikutana nayo kwa viongozi wa chama ngazi ya kata ni ukosefu wa usafiri hivyo anaamini ujio wa pikipiki hizo utasaidia kutatua changamoto hiyo.
Ndugu Mayaya amewarai viongozi hao kuepuka migogoro katika matumizi ya pikipiki hizo na kwa kuwa amekabidhiwa katibu siyo kwamba mwenyekiti hatakiwi kuitumia kwa shughuli za chama bali katibu amekabidhiwa kwa kuwa katiba ya chama inamtaja katibu ndiye mlinzi wa mali za chama.