Wakazi wa Bunda watakiwa kutumia wiki ya sheria kupata uelewa wa sheria
29 January 2024, 2:25 pm
Mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano amewataka wananchi wote wilaya ya Bunda kuitumia wiki ya sheria ili kupata elimu mbalimbali za kisheria.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano amewataka wananchi wote wilaya ya Bunda kuitumia wiki ya sheria ili kupata elimu mbalimbali za kisheria.
Dc Naano ameyasema hayo katika uzinduzi wa wiki ya sheria wilayani Bunda ambayo imefanyika katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Bunda, kauli mbiu mwaka huu ikisema ’’Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa taifa nafasi ya mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai’’.
Naye hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Bunda Mulokozi Paschal Kamuntu amewasihi wakazi wa Bunda kujitokeza katika wiki ya sheria kwa kuwa wapo wataalamu mbalimbali kama vile Jeshi la polisi, Mahakimu, Mawakili, Waendesha mashtaka, Takukuru, miongoni mwa wataalamu wengine.
Aidha Kamuntu amesema kwa sasa wananchi wamebadilika tofauti na zamani hasa katika kuhofia mahakama ambapo zamani ilikuwa vigumu kwa wananchi kusogelea ama mahakama au mahakimu lakini kutokana na huduma kusogea karibu nao wamebadilika.
Kamuntu amesema wataalamu wapo kuanzia tarehe 24 mwezi Jan, na tamati au kilele cha siku ya sheria itakuwa tarehe 1 Feb 2024 katika viwanja vya mahakama ya wilaya mjini Bunda.