Mazingira fm waipa tano TADIO kwa mafunzo
8 July 2023, 1:10 pm
Mtandao wa redio za kijamii Tanzania TADIO waendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka redio za kijamii namna ya kutumia mitandao ili iwe fursa kwao.
Na Catherine Msafiri na Avelina Sulusi
Wito umetolewa kwa viongozi wa redio za kijamii kusimamia waandishi ili mafunzo ya matumizi ya redio mtandao wanayoyapata yasaidie kuleta mabadiliko katika redio zao.
Wito huo umetolewa Julai 7, 2023 na Hilali Alexerder Ruhundwa ambaye ni mhariri wa Radiotadio iliyoko chini ya Mtandao wa Redio za Kijamii Tanzania TADIO wakati akizungumza na Mazingira Fm alipofika kituoni hapo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya namna ya kuchapisha habari katika mtandao, lengo kuu likiwa ni kuziunganisha redio za kijamii zitumie jukwaa hilo kubadilishana habari.
Ruhundwa amebainisha kuwa kutokana na mafunzo wanayotoa wanatarajia kuona radio zinabadilika na kuwa kwenye mitandao ya kijamii lakini pia waandishi wanatumia mwanya huo kama fursa kwao hasa ikizingatiwa teknolojia inabadilika kila siku hivyo waandishi na redio wanalazimika kubadilika kulingana na teknolojia.
Aidha amebainisha kuwa TADIO kama mtandao wa radio za kijamii Tanzania wamelazimika kuanzisha jukwaa la redio mtandao lengo kuu likiwa ni kuziunganisha redio za kijamii zitumie jukwaa hilo kubadilishana habari sanjari na kufikia watu wengi zaidi duniani.
Kwa upande wao waandishi wa habari wa kituo cha Mazingira Fm wameishukuru Tadio kwa mafunzo waliyoyapata na kutokana na mafunzo hayo wamejua namna ya kuchapisha habari kwenye mtandao pia kutumia mitandao ya kijamii kama fursa .
Aidha wameiomba TADIO kuendelea kutoa mafunzo haya ili yaendelee kuwajenga na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.