Jela miaka 30, viboko 12 kwa ubakaji
2 June 2023, 12:07 pm
Mahakama ya wilaya ya Bunda imemhukumu Masubugu Masubugu (32) mkazi wa Bunda mjini kifungo cha miaka thelathini jela na kuchapwa viboko 12 pamoja na kumlipa fidia mhanga kiasi cha shilingi milioni moja kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 13 mwanafunzi wa darasa la saba.
Hukumu hiyo imetolewa Mei 30 mwaka huu katika mahakama ya wilaya ya Bunda mbele ya mheshimiwa Hakim Mkazi Mfawidhi Mulokozi Kamuntu ambapo ni kesi nambari 59/2023.
Ilielezwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa serikali toka jeshi la polisi D/Sgt Athumani Salimu kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo majira ya saa nane mchana eneo la mtaa wa Luselu ndani ya mji wa Bunda ambapo mshtakiwa alimkamata mtoto huyo kwa nguvu na kumwingiza kwenye nyumba ya nyasi kisha kumbaka kwa nguvu.
Baada ya kumaliza tendo hilo la kinyama mshtakiwa alitoka na kukimbilia kusikojulikana.
Mtoto alitoa taarifa kwa wazazi wake na kupelekwa kituo cha polisi kisha hospitali kwa matibabu na uchunguzi.
Athumani alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo huku akijua kuwa ni kinyume na kifungu cha 130 (1) (2) (e) na kifungu Cha 131 (1).
Mwendesha mashtaka aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa kuwa matukio ya kinyama yamekuwa yakikithiri kwenye jamii na kuharibu saikolojia ya watoto ambao ni viongizi wa kesho ili liwe fundisho kwa mshtakiwa na kwa watu wengine wenye tabia kama yake.
Mshtakiwa katika utetezi wake alikiri kutekeleza kitendo hicho na aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa alipitiwa na kuwa shetani ndiye aliyemlaghai.
Baada ya maelezo hayo Mheshimiwa Mulokozi Kamuntu alisema mahakama imejiridhisha pasi na shaka kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo hivyo mahakama inamhukumu kwenda jela miaka 30, kuchapwa 12 na kulipa fidia kwa muhanga kiasi cha shilingi milioni moja.