Nassar: ili tumkomboe mwanamke inabidi tuanze na fikra Uchumi.
8 March 2022, 7:49 am
Halmashauri ya Mji wa Bunda imeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo kidunia huadhimishwa tarehe 08/03/2022.
Katika Maadhimisho hayo, Mgeni rasmi ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Joshua Nassari amewapongeza wanawake wote wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa SAMIA SULUHU HASSAN na kusema kuwa Wanawake ni jeshi kubwa kama walivyoandikwa katika Biblia.
Aidha, Mgeni rasmi ameonesha kuchukizwa kwa baadhi ya vitendo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya watu kwenye jamii yetu dhidi ya wanawake na watoto wa kike. Mheshimiwa Nassari, ametoa wiki moja kwa jeshi la Polisi kuwasilisha mezani kwake orodha ya matukio na mashauri ya ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na watoto wa kike yaliyokwisha ripotiwa hadi sasa.
Hata hivyo, Mheshimiwa Nassari amesema, hatosita kuwachukulia hatua za kisheria makundi yote yanayojihusisha na ukatili huo.
Akiendelea kutoa Hotuba yake, Mheshimiwa Nassari ametoa wito wa hamasa kwa wanawake kujihusisha na shughuli mbalimbali zitakazowaingizia kipato ikiwa ni pamoja na kuingia katika vikundi vya ujasiliamali ili waweza kuwezeshwa na Halmashauri kupitia mikopo ya asilimia 10. Hii itawasaidia kuepuka utegemezi unaopelekea manyanyaso na ukatili.
Katika Maadhimisho hayo, Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda ambae pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mathayo Machiru amesema wanawake wa sasa wamekua wakijitoa sana katika shughuli za uzalishaji mali hasa biashara, ujasiliamali, na kujenga nyumba, hii yote ni kutaka kujikwamua kiuchumi. Mheshimiwa Machiru ameongeza kusema kuwa katika mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, wanawake wameonesha uaminifu mkubwa sana wa kurejesha mikopo hiyo.