TGNP wagawa Radio 100 kwa wananchi wa kata ya Nyambureti Wilayani Serengeti.
21 June 2021, 9:53 am
By Edward Lucas.
Wananchi wa Kata ya Nyambureti, Wilayani serengeti Mkoani Mara, wamelipongeza Shirika la Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP kwa kuwapa msaada wa radio kwa akinamama na wasichana waiishio kwenye mazingira magumu.
Wakizungumza baada ya zoezi hilo la ugawaji wa radio lililofanyika 17 June 2021 katika eneo la shule ya msingi Mabuli, wananchi hao wameipongeza TGNP na kusema kuwa radio hizo zitawasaidia kupata taarifa mbalimbali na kujifunza mambo mengi yanayohusu ukatili wa kijinsia.
Mwajuma Chacha Mwita mkazi wa kijiji cha Mabuli ni miongoni mwa wananchi walionufaika na radio hizo ambapo ameishukuru TGNP kwa kuwagawia radio hizo na kusema kuwa wao kama wanawake itawasaidi kupata taarifa mbalimbali dunia.
“Huu mradi waliotupatia wanawake wametusaidia sana, na sisi tutakuwa tunajiboresha kwa kusikiliza kinachoendelea hapa duniani. Natamani kuyasikiliza mambo ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo yanafanyika kila sehemu kwa pande zote mbili mke na mume” Mwajuma alieleza
Naye Happy Musa mkazi wa kijiji cha Mabuli amesema kuwa “mambo mengi yanatendeka kwa wanawake katika ukatili wa kijinsia na unyanyasaji vilevile”.
Aidha kwa upande wake Afisa Programu TGNP, Jackson Malangalila akiongea baada ya zoezi la ugawaji wa radio na maelekezo ya matumizi ya radio hizo amesema Shirika la TGNP kwa kushirikiana na Shirika la UNFPA limeandaa mpango huo maalumu kwa wanawake yaani akina mama na wasichana ambao wanaishi kwenye mazingira magumu kama ulemavu ili kuwapa nafasi na uwezo wa kupata taarifa na maarifa hasa zinazohusu ukatili wa kijinsia.
“Kwa hiyo rai yangu kwenu ni kwamba mtazitumia vizuri hizo radio kwa ajili ya kukusaidia wewe pamoja na jamii yako, kupitia radio hizo utapata habari, utapata taarifa ambazo zitakusaidia katika maisha yako na jamii yako kwa ujumla kwahiyo rai yangu mzithamini na mzitumie kwa manufaa” alisema Jackson.
Amesema wakati mwingine wanaweza wakarudi tena kuwatembelea wananchi hao ili kujua zaidi kwamba “ulipata radio wakati fulani, labda iko wapi na unaitumiaje”.
Awali akizungumza na wananchi hao mara baada ya kukamilika kwa zoezi la ugawaji wa radio, Afisa Mtendaji wa Kata hiyo ya Nyambureti, Kusaya Makulu amewaonya wananchi hao kutobadilisha malengo ya radio hizo kwa kwenda kuziuza na kubainisha kwamba kwa yeyote atakayefanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.