Mazingira FM

Maafisa, askari wa uhifadhi wapongezwa ulinzi wa faru Tanzania

22 September 2024, 11:30 pm

Katibu tawala Wilaya ya Serengeti Angelina Marco, kwenye maadhimisho siku ya faru duniani, Picha na Adelinus Banenwa

Serikali inategemea sana mapato ya watalii ili kufanya shughuli za maendeleo na miongoni mwa wanyama pendwa kwa watalii ni pamoja na faru.

Na Adelinus Banenwa

Katibu tawala Wilaya ya Serengeti Angelina Marco amewapongeza Maafisa na askari wa uhifadhi kwa kuhakikisha idadi ya faru inaongezeka ukilinganisha na miaka ya 90.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, jana kwenye maadhimisho ya siku ya faru duniani katibu tawala huyo amesema Faru ni miongoni mwa wanyama adimu na wa kipekee ambao wapo katika kundi la wanyama  wakubwa watano wanaopatikana Serengeti.

Viongozi wakitoa hati za pongezi kwa wadau wa uhifadhi kwenye maadhimisho ya siku ya faru duniani, Picha na Adelinus Banenwa

Siku hii imeadhimishwa katika eneo la Fort Ikoma Serengeti sept 22, 2024 ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TANAPA kwa kushirikiana na wadau wengine waliweza kufanya mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kufukuza kuku na mbio za hisani.

Angelina mbali  na kuwapongeza wahifadhi kwa kazi kubwa wanayoifanya pia ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanakuwa sehemu ya utunzaji na uhifadhi wa wanyama hao akibainisha kuwa serikali inategemea sana mapato ya watalii ili kufanya shughuli za maendeleo na miongoni mwa wanyama pendwa kwa watalii ni pamoja na faru.

Sauti ya Katibu tawala Wilaya ya Serengeti Angelina Marco

Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi- TANAPA  Izumbe Msindai, Mkuu wa Kanda ya Magharibi amewapongeza maafisa, askari, na wadau kwa kusaidia na kuchangia kwa ajili ya utunzaji wa faru kwani wameendelea kuongezeka.

Kamishna Msindai amesisitiza ili uhifadhi uwe endelevu na inahitajika staili ya mafiga matatu kwa ajili ya utunzaji wa faru ambayo ni serikali, wadau na wananchi.

Maadhimisho ya siku ya faru duniani ilianzishwa mnamo tarehe 22 Sept 2010 ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa jamii pamoja na kupongeza mambo mazuri yanayofanywa na maaskari na wahifadhi wanaofanya kazi ya kuwatunza wanyama hao.

Sauti ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi- TANAPA  Izumbe Msindai, Mkuu wa Kanda ya Magharibi

Awali akizungumza katika salamu za wadau wa uhifadhi  Dkt Victor Kakengi kutoka TAWIRI amesema shuguli za kibinadamu pamoja na  uwindaji haramu ndivyo vilivyopelekea wanyama hao kupungua kwa kasi sana

Baadhi ya wadau wa uhifadhi katika picha ya pamoja kwenye maadhimisho ya siku ya faru duniani, Picha na Adelinus Banenwa

kwa mujibu wa Dkt Kakengi amesema kwa miaka ya 60s hadi mwanzoni mwa miaka ya 90 Afrika ilikuwa na jumla ya faru 65 elfu huku  Tanzania ikiwa na faru elfu 10 na ndiyo nchi ilikuwa inaongoza duniani kwa kuwa na faru wengi.

Aidha Dkt Kakengi ameongeza kuwa baada ya ubinafsi kwa watu kuongezeka faru hao waliuawa na hatimaye Tanzania ilibakia na Faru wasiyozidi 20 tu hali iliyopelekea serikali kuwekeza kwenye ulindaji wa faru ambapo kufikia mwaka wa fedha uliomalizika Tanzania imeongeza idadi ya faru zaidi ya 230 ikiwa ni zaidi ya malengo ya serikali ambayo yalikuwa ni kufikia faru 205 ifikapo mwezi Dec  2023.

Sauti ya Dkt Victor Kakengi kutoka TAWIRI