Mkurugenzi afunguka sababu ya zahanati ya Kung’ombe kutoanza kazi hadi sasa
13 October 2023, 11:40 am
“Takribani shilingi milioni 16 zinahitajika kufanyia maboresho baadhi ya mambo katika zahanati ya Kung’ombe na kufikia mwezi Disemba 2023 itaanza kutoa huduma”
Na Edward Lucas
Kufuatia kilio cha wananchi wa mtaa wa Kung’ombe Halmashauri ya Mji wa Bunda juu ya zahanati kutoanza huduma hadi sasa, Mkurugenzi wa Mji wa Bunda Emmanuel Mkongo ameeleza sababu zilizokwamisha kuanza kazi kwa kituo hicho.
Akizungumza na Radio Mazingira Fm baada ya kufika ofisini kwake juu ya kilio hicho, Mkongo amesema zahanati haijaanza kazi kutokana na marekebisho kadhaa ambayo hayajakamilika ikiwa ni pamoja na eneo ya kichomea taka zote zitakazokuwa zinazalishwa katika zahanati hiyo.
Amesema kwasasa halmashauri inafanya juhudi za kuhakikisha wanapata fedha ili kukamilisha marekebisho yanayohitajika ambayo yanagharimu takribani shilingi Milioni 16 na kwamba hadi kufikia mwezi Desemba 2023 zahanati hiyo iwe imeanza huduma.
Aidha Mkongo ameongeza kuwa kukamilika kwa zahanati hiyo utasaidia utoaji wa huduma hususani kwa mama na mtoto kwani mara nyingi wazazi huwa wanapata dharura ya kujifungua hivyo kwa kuwepo huduma hiyo itasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto