Mazingira FM

WWF waukingia kifua Mto Mara kuzuia kemikali na vitendo vingine vya uchafuzi

12 September 2023, 11:24 pm

Mkondo wa maji ya Mto Mara eneo la Borenga Serengeti likionesha shughuli za binadamu zinavyochangia mto kupanuka. Picha na Edward Lucas

WWF yaweka mpango wa kupanda miti 44,000 kando kando ya Mto Mara na kuweka alama au bikoni ili kuzuia shughuli za uharibifu katika vyanzo vya maji ya mto huo.

Na Edward Lucas

Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira WWF linatarajia kupanda jumla ya miche ya miti 44,000 kando ya Mto Mara na kuweka bikoni ili kuendelea kulinda na kuhifadhi vyanzo vya mto Mara.

Akizungumzia mpango huo, Eng. Christian Joseph Chonya ambaye ni Mratibu wa Programu za Maji Baridi WWF Tanzania amesema kwasasa wanaendelea na mradi mpya unaofadhiliwa na USAID kuwasaidia wananchi kupanda miti kandokando ya mto na pia kuweka alama au bikoni ili kulinda mipaka ya mto Mara.

Eng. Christian Joseph Chonya akiwa hatua chache kutoka katika mkondo wa mto Mara kijiji cha Borenga Wilaya ya Serengeti

Chonya akiwa katika ukaguzi wa eneo linalotarajiwa kupandwa miti takribani 500 kijiji cha Borenga kandokando ya mto Mara kesho tarehe 13 September 2023 ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya 12 ya siku ya Mto Mara

Amesema wananchi wamekuwa wakiendelea na shughuli mbalimbali katika maeneo ya mto ambayo yamekuwa yakichafua vyanzo vya maji na kuhatarisha usalama wa binadamu na viumbe wengine mfano uchenjuaji wa dhahabu, ukataji miti, kilimo na ufugaji hivyo hatua wanazozichukua ni katika kuhakikisha usalama wa mto Mara.

Eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kupanda miti takribani 500 kando ya Mto Mara kijiji cha Borenga Wilaya ya Serengeti. Picha na Edward Lucas

Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Borenga Wilaya ya Serengeti wameipongeza WWF kwa mpango huo na kuahidi kutoa ushirikiano utakaowezesha kulinda vyanzo vya maji ya Mto Mara