Wachimbaji wadogo wa madini Bunda wafunguka kinachowarudisha nyuma
30 July 2023, 11:46 pm
Wachimbaji wadogowadogo walia kukosa msaada na kulazimika kutumia vifaa duni lakini wakati dhahabu inapopatikana ndipo viongozi wa serikali, mamlaka na wadau wengine hujitokeza kwa ajili ya mgao wa mali.
Na Edward Lucas
Utaratibu wa viongozi, wadau na mamlaka zingine za serikali kujitokeza madini yanapopatikana ikiwa hakuna ushiriki wao katika zoezi la utafutaji na uchimbaji wa madini ni moja kati ya mambo yanayowakwamisha wachimbaji wadogo wa madini.
Hayo yamebainishwa na wachimbaji wadogo wa madini katika eneo la Kazaroho lililopo mtaa wa Nyasana kata ya Kabasa Halmashauri ya Mji wa Bunda wakati wakizungumza na Radio Mazingira Fm katika kipindi cha Duarani.
Mgambi Kebacho Mwita ni mchimbaji na mmiliki wa duara katika eneo hilo amesema alitumia takribani mwaka mmoja kuchimba hadi kuufikia mwamba wa dhahabu kwa kutumia vifaa duni huku akisaidiwa na vijana aliokuwa anawalipa kwa huduma ya chakula kutoka nyumbani
Naye Samsoni au maarufu kama Mzee Madevu amesema wengine wanatelekeza maduara kutokana na kukosa uwezo wa kifedha na vifaa duni katika kutambua eneo sahihi la kuchimba hivyo ameiomba serikali kuhakikisha inawatembelea wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.