Mahindi ya bei nafuu bado hayajatibu uhaba wa chakula Nyatwali
27 July 2023, 6:44 pm
Baada ya serikali kuitikia kilio cha wananchi wa Nyatwali kuhitaji kupata mahindi ya bei nafuu, mambo yamekwenda tofauti kilio kimebadilika.
Na Edward Lucas
Baada ya serikali kupeleka huduma ya mahindi ya bei nafuu kwa wananchi wa Nyatwali wilaya ya Bunda, mapya yaibuka ambapo ndani ya wiki mbili ni tani 2.5 tu ndizo zimechukuliwa kati ya tani 30 za mahindi zilizopelekwa katika eneo hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Radio Mazingira FM wananchi hao wamesema kutokana na kusimamishwa shughuli za uzalishaji mali kwa muda mrefu kwa sasa wanakosa fedha ya kununua mahitaji mbalimbali kujikimu kimaisha hivyo wanaiomba serikali iwape bure au iwakopeshe mahindi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Nyatwali, Ramadhani Misongoma amesema kwa kuwa serikali inaendelea na mpango wa kulitwaa eneo hilo na shughuli za maendeleo kwa wananchi zikiwa zimesimamishwa ingependeza wapewe mahindi ya bure ili wajikimu wakisubiri utaratibu wa serikali kuwahamisha.
Naye mwenyekiti wa mtaa wa Tamau, Asafu Ernest Owiti amesema kuwa baada ya kupokea mahindi hayo yanayouzwa shilingi 920 kwa kilo moja na shilingi 3,680 kwa ‘amboni’ moja, kumekuwa na mapokeo tofauti kutoka kwa wananchi.
Amesema kwa wananchi wa mtaa wa Tamau wakiongeza na gharama ya usafiri kwenda Nyatwali kilipo kituo cha kuuzia mahindi hayo itagharimu takribani shilingi 5,000 kwa thamani ya amboni jambo ambalo wanalazimika kununua katika eneo lao ambapo mahindi ni kati ya shilingi 4,000 kwa ambaoni moja.
Awali akizungumzia hali ya uuzaji wa mahindi katika kituo hicho, Meneja Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Kanda ya Shinyanga, Revocatus Bisama baada ya kutafutwa na Mazingira FM kwa njia ya simu amesema baada ya kupokea ombi la mkuu wa wilaya ya Bunda wamepeleka tani 30 ikiwa lengo ni kupeleka tani 60 lakini hadi kufikia tarehe 25 Julai 2023 walikuwa wameuza tani 2.5 tu ikiwa ni takribani wiki mbili tangu mahindi yafikishwe katika kituo hicho.