Mitaro ya Maji kuongeza ulinzi wa Barabara
5 May 2023, 10:31 am
Wakazi wa kata ya Nyasura Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara wametakiwa kulinda miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha mitaro iko safi ili maji yaendelea kupita vizuri pasipo kuharibu barabara.
Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata hiyo, Mh Magigi Samweli Kiboko wakati akifanya mahojiano na Radio Mazingira Fm jana tarehe 3 May 2023 kuhusu ufanisi wa mitaro katika kuendelea kulinda miundombinu ya barabara hususani katika kipindi hiki mvua zikiendelea kunyesha.
Mh Kiboko amesema hali ya sasa ni afadhali kuliko mwanzoni kwani barabara zilikuwa zikiwekewa changarawe lakini zinaharibika baada ya muda mfupi lakini kwasasa barabara zilizowekewa mitaro zimeendelea kuwa imara licha ya mvua kuendelea kunyesha.
Kwa sasa hivi tangu tumejenga mitaro hii, barabara zile ambazo tumejenga mitaro na kuweka moramu kwa kweli zinapitika kipindi chote wakati mvua inanyesha” alisema Mh Kiboko.
Akitolea mfano wa barabara ya Nyasana, Dr Nchimbi na barabara ya Mabanzini maduka 7 amesema zilikuwa hazipitiki kiurahisi katika kipindi cha mvua kwani maji yalikuwa yakipita juu lakini kwasasa tangu zijengewe mitaro na kuwekewa moramu zinapitika kwa muda wote.
Kwa upande wao baadhi ya wakaazi wa kata ya Nyasura wamethibitisha kuwepo na mabadiliko makubwa katika upitikaji wa barabara hizo kwasasa tofauti na ilivyokuwa mwanzoni licha ya kutaja kasoro ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na baadhi ya mitaro kuwa mifupi na kuruhusu maji kupita juu ya barabara na kukosekana kwa moramu zinapitika kwa muda wote.
Picha kutoka maktaba yetu zilizopigwa miaka 4 iliyopita mtaa wa Nyasura ‘D’ zikionesha uharibifu mkubwa wa barabara wakati wa msimu wa mvua kutokana na kukosekana mitaro ya kupitisha maji.