Wakaazi elfu 7,000 kunufaika na mradi wa maji Misisi-Zanzibar katika Halmashauri ya Mji wa Bunda.
3 March 2023, 2:39 pm
Zaidi ya watu 7,000 ambao ni wastani wa kaya 1000 wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji wa Misisi-Zanzibar katika Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji Bunda BUWASA, Esther Gilyoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji wa Bunda mkutano wa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023 uliofanyika jana tarehe 2 March 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Bi.Esther amesema BUWASA ilianza utekelezaji wa mradi huo tangu mwezi Novemba 2022 na hadi kufikia tarehe 28 Feb 2023 mradi umekamilika na kuanza kufanya kazi, hivyo amewaomba wananchi kujiunga na huduma hiyo ya maji ili kuondokana na changamoto waliokuwa wanakumbana nayo.
Katika hatua nyingine Bi Esther amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 inatarajia kukamilisha miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa Manyamanyama-Mgaja na Balili-Kunzugu huku ikiwa na matarajio ya kutekeleza miradi mikubwa miwili katika mji wa Bunda kwa mwaka wa fedha 2023/2024.