Mazingira FM

Wakazi wa Kisangwa Bunda walia na choo mnadani.

1 March 2023, 3:48 pm

Wakaazi wa Kisangwa kata ya Mcharo Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara wamelalamikia ukosefu wa huduma ya choo katika mnada wa Kisangwa jambo linalohatarisha usalama wa afya zao.

Wakizungumza na Radio Mazingira Fm  wamesema kukosekana kwa usimamizi katika choo kilichojengwa katika maeneo hayo, imechangia kukithiri kwa uchafu jambo lililopelekea choo hicho kuchakaa na kutoendelea kutumika.

 Wamesema baadhi ya watu wanaofika katika mnada huo kwa ajili ya mahitaji mbalimbali wamekuwa wakijisaidia hovyo katika maeneo hayo hali inayopelekea kuhatarisha afya zao.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sengerema unakopatikana mnada huo, Gabriel Mwita Marwa amesema changamoto inayoukabiri mnada huo ni suala la usafi ambapo awali asimilia 20 ya mapato ya mnada yalikuwa yanatengwa kwa ajili ya kata hiyo lakini tangu mpango huo uondolewe na halmashauri kuchukua asimilia 100 ya mapato suala la usafi limekuwa ni changamoto.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Kisangwa ambaye pia anakaimu mtaa wa Sengerema, Jainesi Majogoro amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kwamba tayari amekwisha awasilisha katika ngazi za juu kwa utekelezaji zaidi.