Mazingira FM

Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Joshua Nassari amezindua mradi wa maji katika shule ya Msingi Kabirizi

16 December 2022, 8:20 am

Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Joshua Nassari amezindua mradi wa maji katika shule ya Msingi Kabirizi iliyopo katika Kata ya Nampindi.

Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 14/12/2022.
Mhe. Mkuu wa Wilaya alianza kwa kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Rais Dr. Samia Suluhu kwa kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo hapa nchini.

Mkuu huyo wa Wilaya aliwaeleza wananchi kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja serikali imepeleka jumla ya shilingi 756,392,379.85 katika Kata ya Nampindi pekee yake.. Fedha hiyo ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizindua mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Bunda amewataka wananchi kuhakikisha kuwa wanalinda miundombinu ya mradi huo kwani ni fedha nyingi zimewekezwa katika mradi huo.

 

Mkuu huyo wa Wilaya Mhe. Joshua Nassari pia amepiga marufuku wavuvi kupitisha mitumbwi na boti katika eneo ilipowekwa pampu ya maji. “Natangaza marufuku kuanzia leo, hakuna mtumbwi au boti kupita eneo hili”

Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bi. Restuta Saasita aliwataka wananchi wanaozunguka eneo hilo la mradi kuwa walinzi wa miundombinu ya mradi huo kwa kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu uendeledvu wa mradi huo.

Awali akisoma taarifa ya utelelezaji wa mradi huo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Msingi Mwalimu Chekanao Mwandumbya ameeleza kuwa fedha za mradi huo wa EP4R zilipokelewa katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Fedha zilizopokelewa ni shilingi 31,892,379.85, fedha zilizotumika hadi kukamilisha mradi huo ni shilingi 29,204,600.00 na hivyo shilingi 2,167,779.85 zimebaki ambazo zitatumika katika uendelezaji wa mradi huo.

Naye Diwani wa Kata ya Nampindi Mhe. Fedson Rwesunga ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwekeza fedha nyingi za miradi katika Kata ya Nampindi na hivyo kuwasisitiza wananchi kuhakikisha wanathamini na kuitunza miradi hiyo ukiwemo mradi huo wa maji.

 

Aidha Mhe. Rwesunga amempongeza Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kabirizi kwa usimamizi mzuri wa miradi katika shule yake. “Huwa pesa ikiingia shule ya msingi Kabirizi napata usingizi kwani sina shaka na uwajibikaji wa Mwalimu huyu”