Mazingira FM
Mazingira FM
23 November 2025, 7:51 pm

Mamlaka hiyo ya maji inakwenda kutatua changamoto kubwa ya maji inayokabili chuo hicho na jamii ya wakazi wa kisangwa kwa muda mrefu.
Na Adelinus Banenwa
Kiasi cha shilingi milioni moja na laki nane kimepatikana katika mahafali ya 41 chuo cha Maendeleo ya wananchi kisangwa. Fedha hizo zimepatika zikilenga kutatua changamoto ya nishati ya kusomea kwa wanafunzi chuoni hapo pale umeme unapokatika.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo Bi Esther Gilyoma ambaye ni Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bunda BUWSSA amechangia kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano huku wageni wengine wakichangia shilingi laki tatu.
Aidha katika hatua nyingine Bi Gilyoma amesema mamlaka hiyo ya maji inakwenda kutatua changamoto kubwa ya maji inayokabili chuo hicho na jamii ya wakazi wa kisangwa kwa muda mrefu

Amesema serikali tayari imetoa kiasi cha shilingi milioni 700 ambapo tayari kazi ya kufikisha maji kisangwa inaendelea ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba huku akihakikishia jamii ya wanafunzi wa kisangwa kuwa suala la changamoto ya maji inakwenda kuwa historia.

Awali Frances Kusekwa mkuu wa chuo cha Kisangwa akisoma taarifa ya chuo amesema chuo hicho kinaendelea kuwa msaada mkubwa sana kwa vijana kupata ujuzi unaowasaidia kujiajiri au kuajiriwa katika sekta za uzalishaji mali.
Kusekwa amesema pamoja na mafanikio makubwa ya chuo hicho ikiwemo ukarabati wa majengo, kuongezwa kwa vifaa vya kujifunzia, kuongeza udahili wa wanafunzi, bado zipo changamoto mbalimbali zinazikikabili chuo hicho.
Kupitia risala ya wahitimu wa chuo hicho wamebainisha changamoto hizo ikiwa ni pamoja na upungufu wa mabweni kwa jinsi zote, upungufu wa vifaa vya kujifunzia, changamoto ya maji safi na salama, tatizo la ubora wa barabara iendayo chuoni, upungufu wa watumishi miongoni mwa changamoto zingine.