Mazingira FM
Mazingira FM
25 October 2025, 8:53 pm

Waliopoteza vitambulisho vyao vya kupigia kura na majina yao yapo kwenye daftari la kudumu la mpiga kura wanayo nafasi ya kupiga kura kwa kutumia vitambulisho vyenye majina yao kama vile leseni ya udereva pass ya kusafiria au kitambulisho cha taifa yaani NIDA.
Na Adelinus Banenwa
Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Mwibara na jimbo la Bunda halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara Oscar Jeremah Nchemwa amesema maandalizi yote kuelekea uchaguzi mkuu 2025 katika majimbo hayo yanaendelea vizuri na hakuna changamoto yoyote.
Akizungumza katika kipindi cha ufahamu wa sheria kinachorushwa na Mazingira FM amesema katika majimbo yote kuna jumla ya vituo vya kupigia kura 384 na kati ya hivyo jimbo la Bunda lina vituo 161 na jimbo la Mwibara lina jumla ya vituo 223 huku wapiga kura wenye sifa katika majimbo yote mawili ni 143,315.
Nchemwa ameongeza kuwa kwa wale wapiga kura ambao wamepoteza vitambulisho vyao vya kupigia kura na majina yao yapo kwenye daftari la kudumu la mpiga kura wanayo nafasi ya kupiga kura kwa kutumia vitambulisho vyenye majina yao kama vile leseni ya udereva, pass ya kusafiria au kitambulisho cha Taifa yaani NIDA.
Amewatoa hofu wananchi kuhusu hali ya usalama katika vituo vya kupigia kura katika majimbo yote mawili kwa kuwa tayari wasimamizi wa uchaguzi wanashirikiana vyombo vya usalama kuhakikisha usalama unakuwepo kwenye vituo.