Mazingira FM
Mazingira FM
26 September 2025, 6:55 pm

Jumla ya wanafunzi 291 kati ya wanafunzi 374 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2022.
Na adelinus Banenwa
Jumla ya wanafunzi 291 wamehitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Migungani mwaka 2025. Kati ya idadi hiyo, wanafunzi wa kike ni 159 na wavulana 132. Wahitimu hao ni sehemu ya wanafunzi 374 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2022.
Wakisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi katika mahafali ya pili tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2021, wanafunzi hao wamesema kuwa wanafunzi 83 hawakumaliza masomo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro na baadhi yao kuhamia shule nyingine.

Katika risala hiyo, wahitimu walitaja changamoto zinazokabili shule hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa jiko la kupikia chakula, uhaba wa matundu ya vyoo, upungufu wa walimu pamoja na baadhi ya madarasa kukosa umeme licha ya kuwepo kwa huduma ya umeme shuleni hapo.

Wamesema changamoto ya ukosefu wa jiko pamoja na kutokuwepo kwa umeme kwenye madarasa ni vipaumbele vinavyopaswa kushughulikiwa haraka kwa ajili ya ustawi wa wanafunzi waliopo na wanaotarajiwa kujiunga na shule hiyo.

Akijibu risala hiyo, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Ndugu Peter Charles ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Pamba ya 4C, amesema yeye pamoja na wageni waalikwa wamekusanya jumla ya shilingi milioni moja laki sita na themanini na tatu elfu.
Amesema fedha hiyo itatumika kuweka umeme kwenye madarasa yote pamoja na kuanza mchakato wa ujenzi wa jiko la kudumu shuleni hapo, huku akiwataka wadau wengine kuendelea kushirikiana na shule hiyo katika kuboresha mazingira ya kujifunzia.