Mazingira FM
Mazingira FM
11 September 2025, 8:36 pm

Maadhimisho hayo ya 14 yanatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 15, 2025, katika Viwanja vya Mwenge, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.
Na Thomas Masalu
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho ya ‘Mara Day’ yanayoshirikisha nchi za Tanzania na Kenya.
Maadhimisho hayo ya 14 yanatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 15, 2025, katika Viwanja vya Mwenge, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 11, 2025, ofisini kwake mjini Musoma, Kanali Mtambi amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa wakazi wa Mkoa wa Mara kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo mkoani humo, zikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Bonde la Mto Mara.
Aidha, Kanali Mtambi ameeleza kuwa shughuli mbalimbali zimeandaliwa kufanyika katika maadhimisho hayo, zikiwemo zoezi la upandaji wa miti takribani 8,000 katika Kijiji cha Kirumi, Wilaya ya Butiama, maonesho ya teknolojia mbalimbali zinazotumika katika uhifadhi wa mazingira, na michezo ya kuhamasisha ushiriki wa jamii.
Kadhalika, elimu ya uhifadhi wa Mto Mara itatolewa kwa vijiji 136 vinavyopakana na bonde hilo, kwa lengo la kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika kulinda mazingira.