Mazingira FM

Wanafunzi 66,102 kuhitimu elimu ya msingi Mara

10 September 2025, 7:42 am

Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara, Bulenga Makwasa

Maandalizi yote ya mtihani huo yamekamilika kwa ufanisi, na kufikia jana mitihani yote ilikuwa tayari imesambazwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Mara.

Na Adelinus Banenwa

Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara, Bulenga Makwasa, amesema jumla ya wanafunzi 66,102 kutoka shule za msingi 911 za mkoa huo wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba kuanzia tarehe 10 hadi 11 Septemba mwaka huu, 2025.

Akizungumza na Mazingira FM, Makwasa amesema kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 31,515 na wasichana ni 34,587. Aidha, kusimamia zoezi hilo la kitaifa, jumla ya wasimamizi 4,839 wameteuliwa na kupelekwa katika vituo mbalimbali vya mitihani mkoani humo.

Afisa elimu huyo ameongeza kuwa maandalizi yote ya mtihani huo yamekamilika kwa ufanisi, na kufikia jana mitihani yote ilikuwa tayari imesambazwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Mara bila changamoto yoyote.

Makwasa amewatakia kila la heri wanafunzi wote wanaokabiliwa na mtihani huo, huku akiwataka kujiamini na kutumia maarifa waliyopata darasani ili kufanikisha malengo yao ya kitaaluma.

Sauti ya Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara, Bulenga Makwasa,

Amehitimisha kwa kutoa rai kwa wanafunzi kujiepusha na udanganyifu wa aina yoyote, akisisitiza kuwa kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, Mkoa wa Mara umekuwa mfano wa kuigwa kwa kutokuwa na kisa chochote cha udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.