Mazingira FM
Mazingira FM
9 September 2025, 10:10 pm

Amewasihi wazazi kushirikiana na walimu katika kuhakikisha watoto wanapata maandalizi bora ya mtihani, ikiwa ni pamoja na kuwaandalia mazingira tulivu ya kujisomea na kupumzika.
Na Adelinus Banenwa
Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Salumu Mtelela, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Aswege Enock Kaminyoge, amewataka walimu, wanafunzi pamoja na wasimamizi wa mitihani kujiepusha na aina yoyote ya udanganyifu katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba unaotarajiwa kufanyika tarehe 10 na 11 Septemba, mwaka huu.
Akizungumza na Radio Mazingira fm leo 9 SEPT 2025 Mtelela amesema wanafunzi kwa maaana ya wahitimu, walimu pamoja na wasimamizi wanatakiwa kuzingatia sheria za baraza la mitihani ili kuepuka masuala ya udanganyifu katika mtihani huo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, jumla ya wanafunzi 13,075 wanatarajiwa kufanya mtihani huo katika Wilaya ya Bunda. Kati yao, 4,951 wanatoka Halmashauri ya Mji wa Bunda, wakiwemo wavulana 2,337 na wasichana 2,614, huku 8,124 wakitoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, wavulana wakiwa 4,162 na wasichana 3,962.
Aidha, amewasihi wazazi kushirikiana na walimu katika kuhakikisha watoto wanapata maandalizi bora ya mtihani, ikiwa ni pamoja na kuwaandalia mazingira tulivu ya kujisomea na kupumzika.
Mtelela amehitimisha kwa kuwatakia wanafunzi wote kila la heri katika mtihani huo, akiwataka kuwa na moyo wa ujasiri na kutojihusisha na udanganyifu wa aina yoyote.