Mazingira FM

Bunda: Fundi aliyekwama duarani apatikana akiwa amefariki

21 August 2025, 11:12 pm

Picha ikionesha hali ya shimo la uchimbaji alimokwamia fundi kabla ya kufumuliwa ili kuendelea na zoezi la kumuokoa

Na Edward Lucas.

Juma Lutamula (33), mchimbaji katika mgodi wa Walwa uliopo katika machimbo ya Kinyambwiga, amepatikana jioni ya leo akiwa tayari amefariki baada ya kufukiwa na kifusi wakati akifanya kazi ya ujenzi wa duara la uchimbaji.

Lutamula alipata ajali hiyo tangu juzi, tarehe 19 Agosti 2025, majira ya saa 12 jioni, na juhudi za uokoaji zilianza mara moja hadi leo jioni walipofanikiwa kuupata mwili wake ukiwa takribani futi 80 ndani ya duara alilokuwa akifanyia kazi.

Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Augustine Magere, amethibitisha kupatikana kwa mwili wa Lutamula, na kutoa wito kwa wachimbaji kuzingatia usalama hasa kufanya ukaguzi wa maduara kabla ya kuanza kuyatumia.

Augustine Magere

Kwa upande wake, mkaguzi wa mgodi huo, Juma Mashauri, ameeleza kuwa jitihada za uokoaji zilichukua muda mrefu kutokana na ugumu wa kazi, na ameishukuru timu ya zimamoto pamoja na wachimbaji wote walioshiriki zoezi hilo.

Juma Mashauri

Mwili wa Lutamula umepelekwa chumba cha kuhifadhia mwili hospitali ya DDH Bunda kwa ajili ya maandalizi ya taratibu zingine za mazishi