Mazingira FM

Dereva fika polisi ndani ya saa 12 baada ya kusababisha ajali

13 August 2025, 7:07 pm

ASP Faustin .J. Buhembere Mkuu wa Usalama barabarani wilaya ya Bunda

Mazingira ya dereva kukimbia eneo la tukio la ajali linashauriwa endapo mazingira ya usalama wake yatakuwa ni hatari na si vinginevyo.

Na Adelinus Banenwa

Imeelezwa kuwa kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani kifungu cha 68 kinamtaka dereva aliyesababisha ajali  kuripoti kituo cha polisi ndani ya saa kumi na mbili 12

Hayo yamesemwa na ASP Faustin .J. Buhembere ambaye ni Mkuu wa Usalama barabarani wilaya ya Bunda wakati akizungumza na wananchi kupitia Radio Mazingira FM kwenye kipindi cha Asubuhi leo ambapo amesema mazingira ya dereva kukimbia eneo la tukio la ajali linashauriwa endapo mazingira ya usalama wake yatakuwa ni hatari na si vinginevyo.

ASP Faustin .J. Buhembere Mkuu wa Usalama barabarani wilaya ya Bunda akiwa na A/ISP Emmanuel Joseph ambaye pia ni mkuu wa usalama barabarani msaidizi wilaya ya Bunda

Aidha Buhembere amesema ikiwa mazingira si hatari kwa dereva anatakiwa kusimama, kutoa taarifa kituo cha polisi , kusaidia shughuli za maokozi, na kuhakikisha haondoi chombo kwenye eneo la ajali.

Sauti ya ASP Faustin .J. Buhembere Mkuu wa Usalama barabarani wilaya ya Bunda

Naye mkaguzi msaidizi wa polisi Emmanuel Joseph ambaye pia ni mkuu wa usalama barabarani msaidizi wilaya ya bunda amesema mbali na wajibu aliyonao dereva pia wananchi wanao wajibu wa kutoa msaada kwa wahanga, kutoa ushahidi namna ajali ilivyotokea, kulinda eneo la ajali kutoa taarifa kituo cha polisi pamoja na kuepuka kujichukulia sheria mkononi ikiwepo kumshambulia dereva.

A/ISP Emmanuel Joseph mkuu wa usalama barabarani msaidizi wilaya ya Bunda

Emmanuel ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi la pilisi pia kuzingatia elimu ya usalama barabarani inayoendelea kutolewa ili kuwa na usalama wakati wote wa matumizi ya barabara.

Sauti ya A/ISP Emmanuel Joseph mkuu wa usalama barabarani msaidizi wilaya ya Bunda