Mazingira FM
Mazingira FM
10 August 2025, 3:20 pm

“Ukiwa mdau wa maendeleo na ukatoa mchango unaoigusa jamii moja kwa moja basi na wewe mungu anazidi kukubariki”
Na Taro Michael Mujora
Wadau mbalimbali wametakiwa kushirikiana kwa karibu na jamii katika kugusa mahitaji ya watu wenye uhitaji, hususan kupitia taasisi za kijamii kama makanisa, ili kujenga mshikamano na kuleta maendeleo ya pamoja.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Janeth Motors Company Limited, Bi. Janeth Webiro akiwa mgeni rasmi katika hafla ya changizo iliyofanyika katika Kanisa la AICT Changuge kata ya Mcharo Wilaya ya Bunda, ambapo kampuni hiyo imekabidhi vifaa vya muziki pamoja na msaada wa shilingi 300,000 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kanisa na kazi za injili.
Aidha, asema kuwa ni kwa kushirikiana tu ndipo jamii inaweza kupiga hatua na kuwajumuisha wale walioko pembezoni katika maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Meneja wa kampuni hiyo, Bw. Waiter Natey, amesema kuwa mchango huo ni sehemu ya kujenga mshikamano wa kijamii na kuunga mkono jitihada za makanisa katika maendeleo ya jamii
Viongozi wa Kanisa la AICT Changuge wamesema kuwa vifaa hivyo vya muziki vitasaidia katika kuimarisha ibada, kazi za uinjilisti, na kuvuta waumini wengi zaidi, huku wakitoa shukrani kwa wote waliounga mkono hafla hiyo.
Hafla hiyo ya changizo iliandaliwa na Idara ya Wanawake kutoka makanisa ya AICT Changuge, Kisangwa, Mirungu na Bukore yaliyopo kata ya Mcharo, ikiwa na lengo la kukusanya michango kwa ajili ya maendeleo ya kanisa na kuimarisha huduma zake kwa jamii.