Mazingira FM
Mazingira FM
19 July 2025, 7:23 pm

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa kijana huyo aliuawa kwa kunyongwa.
Na Adelinus Banenwa
Kijana Yusto Kungu dereva bodaboda aliyekutwa ameuawa amezikwa leo nyumbani kwao katika kijiji cha Nyasirori, wilayani Butiama , mkoani Mara.
Yusto alikuwa mwendesha pikipiki maarufu kama bodaboda katika kijiwe cha NM Bunda aliyepotea baada ya kubeba abilia na baadaye mwili wake ulipatikana ukielea katika maji ya Ziwa Victoria katika kijiji cha Bugwema, halmashauri ya wilaya ya Musoma
Kwa mujibu wa kiongozi wa kijiwe cha NM, Yusto alichukuliwa na watu watatu siku ya Jumapili kwa makubaliano ya kuwapeleka Busekela kwa malipo ya shilingi 30,000.
Tangu siku hiyo hakuonekana tena hadi mwili wake ulipopatikana Julai 18, licha ya juhudi za kumtafuta zilizofanywa na familia na wafanyakazi wenzake.

Ndugu wa marehemu Yusto , Ezron Benjamin, amesema familia ilipata taarifa za kutoweka kwake kupitia kwa mke wake, na baadaye wakaanza msako kwa kushirikiana na waendesha bodaboda wenzake. Hadi july 18 walipopata taarifa kupitia kwa mvuvi aliyekuwa akivua samaki kandokando ya ziwa alipotoa taarifa za uwepo wa mwili wa mtu ziwani ukielea.
Yusto ameacha mjane, Aidha familia yake imesema kuwa bado haijulikani mahali ilipo pikipiki ya marehemu, na wameomba haki itendeke kwa kuwatia mbaroni waliohusika na mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, SACP Pius Lutumo, amethibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa kijana huyo aliuawa kwa kunyongwa. Polisi wamefungua jalada la kesi na wanaendelea kuwasaka wahusika wa tukio hilo.