Mazingira FM

Bunda TC yapewa kongole hati safi ripoti ya CAG

13 June 2025, 4:07 am

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi, Kwenye kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya mji wa Bunda

Mhe. Mtambi ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi na kuwa na hoja chache za ukaguzi ukilinganisha na Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mara ambazo zinahoja nyingi.

Na Thomas Masalu

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo juni 13, 2025 katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi na kuwa na hoja chache za ukaguzi ukilinganisha na Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mara ambazo zinahoja nyingi.

sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi

Pamoja na pongezi hizo Mhe. Mtambi amelitaka Baraza la Madiwani kuisimamia Halmashauri kuandaa mpango mkakati wa kutekeleza maagizo matatu yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Fedha za Serikali za Mitaa (LAAC) na hoja zilizobakia za ukaguzi.

sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi

Akiwasilisha taarifa yake, Mwekahazina wa Halmashauri ya Mji wa Bunda CPA Antonia Ndawi amesema Halmashauri ya Mji wa Bunda katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2023/2024 imepata hati safi kwa taarifa zote tatu yaani taarifa ya ujumla, mfuko wa pamoja wa afya, na mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mkuu wa mkoa wa Mara Mhe.Evans Mtambi akiwa na mkuu wa wilaya ya Bunda Mh.Aswege Kaminyoge (kulia kwake) na viongozi mbalimbali,(picha na Thomas Masalu)

CPA Ndawi amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ilikuwa na hoja 21 na kati ya hoja hizo hoja 16 zimetokana na taarifa ya jumla, hoja nne zimetokana na mfuko wa pamoja wa afya na hoja moja ya mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kati ya hoja hizo tano zimejibiwa na kushafungwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Mhe. Michael Kweka amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Marakwa ushirikiano wake alioutoa katika Baraza hilo na kushukuru ushirikiano kati ya madiwani, menejimenti na watumishi wa Halmashauri hiyo.

mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Mhe. Michael Kweka

Kikao hicho kilihudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Bunda, baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Madiwani na Menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Bunda.