

12 February 2025, 10:53 pm
Kati ya walimu 350 waliopo halmashauri ya wilaya ya Bunda walimu wa kike ni 45 pekee.
Na Edward Lucas
Kutokana na kilio cha kukosa mwalimu wa kike shule ya sekondari Tirina, mkuu wa wilaya ya Bunda, Dr Vicent Naano Anney amempa siku moja mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo awe amempa barua ya kuonesha mwalimu amepelekwa katika shule hiyo
Naano ametoa maagizo hayo leo kupitia mkutano wa baraza la madiwani kupokea taarifa mbalimbali ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 katika halmashauri ya wilaya ya Bunda
Awali akizungumzia changamoto hiyo diwani wa kata ya Mugeta, Mganga Jongora amesema shule ya sekondari Tirina ina wanafunzi wa kike na wa kiume lakini toka shule hiyo ifunguliwe haina mwalimu wa kike jambo linalosababisha wanafunzi wa kike wakose mtu wa kumfikishie changamoto zao
Katika mahojiano na Mazingira Fm, Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, Nambua Godfrey Semlugu amekiri kuwepo changamoto ya uhaba wa walimu wa kike kwani kati ya walimu 350 wa kike ni 45 pekee.