Mmoja mbaroni tuhuma za kuhusika na uharibifu wa makaburi Bunda
22 January 2025, 6:00 pm
Hadi sasa amekamatwa mtu mmoja kwa tuhuma hizo za kuharibu makaburi na tayari ameshafikishwa jeshi la polisi.
Na Adelinus Banenwa
Baadhi ya vyuma vinavyodaiwa kung’olewa kwenye makaburi ya Zanzibar vyakamatwa kwenye godauni la vyuma Chakavu Bunda.
Nyabatuli Ndege mwenyekiti wa mtaa wa Zanzibar amesema wakati wakiendelea na jitihada za kuwasaka wahusika wa tukio hilo walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kwamba vyuma hivyo yaani strips vimeonekana katika moja ya godauni la vyuma chakavu katika mtaa wa Manyamanyama mbugani hivyo walichukua hatua za haraka kwenda eneo la tukio na tayari mtu mmoja anashikilowa.
Mtendaji wa Kata ya Nyasura Bi Jerymery Atanasio Kamugisha amesema hadi sasa amekamatwa mtu mmoja jina limehifadhiwa kwa tuhuma hizo za kuharibu makaburi na tayari ameshafikishwa jeshi la polisi.
Bi Jerymary amesema mtuhumiwa huyo amekutwa kwenye godauni lake la vyuma chakavu ana strips ambazo zinaaminika kutoka kwenye makaburi hayo takribani kilo 33.5 hivyo amewatoa hofu wananchi na kusema wale wote waliohusika na uharibifu huo serikali itawakamata na kutawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Baadhi ya ndugu waliohifadhi wapendwa wao katika makaburi hayo ya Zanzibar wameiomba serikali kujenga uzio katika makaburi hayo ili kuimarisha usalama katika eneo hilo au wawaruhusu kuzika majumbani ili kuepuka fedheha kama hiyo iliyotokea.