Zaidi ya makaburi 50 yaharibiwa na watu wasiojulikana Bunda
22 January 2025, 9:49 am
Makaburi yenye vigae ( marumaru ) na mikanda ( strips) ndiyo yanaonekana kulengwa zaidi.
Na Adelinus Banenwa
Katika hali isiyo ya kawaida zaidi ya makaburi 50 yaliyopo mtaa wa Zanzibar kata ya Nyasura Halmashauri ya mji wa Bunda yamevunjwa na kuharibiwa.
Tukio hilo la aina yake limetajwa kufanyika kati ya tarehe 19 na 20 mwezi Jan 2025 ambapo makaburi yenye vigae ( marumaru ) na mikanda ( strips) ndiyo yanaonekana kulengwa zaidi.
Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Zanzibar wakizungumza na redio Mazingira fm wamewatupia lawama wale wanaojihusisha na wauzaji na wanunuzi wa vifaa chakavu kwamba ndiyo kichocheo cha matukio hayo.
Baadhi ya viongozi wa kata ya Nyasura akiwemo Mtendaji wa kata hiyo Bi. Jerymary Atanasio Kamugisha pamoja na diwani wa kata hiyo Mhe. Magigi Samweli Kiboko, wameonesha kusikitishwa kwa tukio hilo huku wakihaidi wale wote waliohusika na tukio hilo kutafutwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.