Mazingira FM

Ofisi ya DC Bunda, Maboto watoa mkono wa pole kwa wahanga wa moto

6 January 2025, 7:23 pm

Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela katikati, Emmanuel Kija katibu wa Mbunge wa jimbo la Bunda mjini kulia wakikabidhi kiasi cha fedha kama mkono wa pole kwa waathirika wa moto

Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bunda kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto imetoa mkono wa pole wa shilingi laki tano 500,000 kwa waathirika wa kuunguliwa na nyumba kata ya Bunda stoo mjini Bunda.

Na Adelinus Banenwa

Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bunda kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge jimbo la Bunda mjini Mhe Robert Chacha Maboto imetoa mkono wa pole wa shilingi laki tano 500,000 kwa waathirika wa kuunguliwa na nyumba mtaa wa miembeni kata ya Bunda stoo mjini Bunda.

Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bunda leo Jan 6, 2025 amewatia moyo takribani kaya 6 zilizoathirika na moto ulioteketeza nyumba waliyokuwa wakiishi ambapo amesema serikali wilayani Bunda tayari imechukua hatua za kuhakikisha Bunda inapata kituo cha zimamoto na uokoaji.

Sauti ya Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela

Mtelela amesema tayari jengo la kuweka kituo cha zimamoto na uokoaji limeshatengwa hivyo kinachosubiliwa kwa sasa ni bajeti itakayowezesha kupatikana rasilimali watu watakaokaa katika ofisi hizo huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari katika matunizi ya vifaa vya moto wakati wa kupika.

Sauti ya Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela
Emmanuel Kija katibu wa Mbunge wa jimbo la Bunda mjini

Emmanuel Kija katibu wa Mbunge wa jimbo la Bunda mjini amesema Mhe Robert Maboto amepokea kwa masikitiko tukio la wananchi kuunguliwa na mali zao ambapo kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya wamekabidhi kiasi cha shilingi laki tano 500,000 ikiwa ofisi ya mbunge imetoa shilingi laki mbili na ofisi ya mkuu wa wilaya ikitoa laki tatu kwa wahanga hao.

Sauti ya Emmanuel Kija katibu wa Mbunge wa jimbo la Bunda mjini
Mohamed Liangwike mkaguzi msaidizi wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara ambaye ndiye mkuu wa operation

Mohamed Liangwike mkaguzi msaidizi wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara ambaye ndiye mkuu wa operation amesema wao kama zimamoto wamefika kubaini chanzo cha moto huo huku wakitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za matukio ya moto kwa haraka tu punde tu tukio linapotokea ili kushiriki kuidhibiti.

Pia Liangwike amesema kutokana na wilaya ya Bunda hasa mji wa Bunda kukua kwa kasi haipingiki kwamba kinahitajika kituo cha zimamoto na uokoaji kilicho na askari na vifaa kamili vya kazi ili kutoa elimu pia kukabiliana na majanga ya maokozi pindi yanapotokea

Sauti ya Mohamed Liangwike mkaguzi msaidizi wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara
viongozi wakikagua sehemu ya mabaki ya nyumba iliyoteketea kwa moto ili kubaini chanzo cha moto huo

IKUMBUKWE, mnamo January  1, 2025 majira ya saa nne na nusu usiku zaidi ya watu 20 katika mtaa wa miembeni kata ya Bunda stoo halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara walinusurika kifo baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto ambapo hadi sasa chanzo cha moto huo bado hakijafahamika.