Bunda mji yazindua vitabulisho vya machinga
27 November 2024, 8:13 am
Wanaofanyabiashara kando ya barabara wanatakiwa kutoka hasa ukizingatia uwepo wao kwenye maeneo hayo ni hatari kwa usalama wao.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano azindua vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo maalufu kama machinga huku akiwataka walioko barabarani kuhama haraka.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe Naano amesema vitambulisho hivyo vya wajasiriamali vina faida kubwa kwao ambapo mfanyabiashara mwenye kitambulisho hicho atapata faida ya kukopa fedha benki ambapo riba yake ni asilimia 7 tu ya mkopo ambapo serikali imeshatoa kiasi cha shilingi 18 bilion kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
Dc Naano ameongeza kuwa kwa wale wanaofanyabiashara kando ya barabara wanatakiwa kutoka hasa ukizingatia uwepo wao kwenye maeneo hayo ni hatari kwa usalama wao.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo ( machinga) mkoani Mara Ndugu Charles Waitara amesema hatua ya serikali kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo ni jambo la kupongezwa kwa kuwa litasaidia kuondoa malalamiko ya wajasiriamali wadogo ya kuombwa kulipa kodi TRA angali mitaji yao ni mdogo, kushindwa kupata fursa za mikopo kwenye taasisi za kifedha kama benki miongoni mwa changamoto zingine.
Naye Maliki afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya mji wa Bunda amesema utaratibu wa kupata kitambulisho cha ujasiriamali ni lazima awe amesajiliwa kwa namba ya NIDA kwenye ofisi za maendeleo ya jamii kwa mkurugenzi wa halmashauri au ofisi za watendaji wa kata.
Maliki ameongeza kuwa baada ya mfanyabiashara kusajiliwa atapewa namba maalumu ya malipo ambapo atalipa kiasi cha shilingi elfu 20 na malipo hayo yatadumu kwa miaka mitatu tofauti na kile cha zamani ambacho kilikuwa kinadumu kwa mwaka mmoja.