Mazingira FM

‘Wakurugenzi wa halmashauri pimeni maeneo ya wafugaji kuondoa mogogoro’

23 August 2024, 3:12 pm

Mwenyekiti wa wafugaji taifa ndugu Mrida Mshota, Picha na Adelinus Banenwa

Wakurugenzi tengeni na pimeni maeneo ya malisho ili kuondoa migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Na Adelinus Banenwa

Wito umetolewa kwa Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kutenga na kupima maeneo ya wafugaji ili kuondoa migogoro baina ya wakulima na wafugaji iliyokuwa imezoeleka.

Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa wafugaji taifa ndugu Mrida Mshota wakati akizungumza na mazingira fm leo Augost 23,2024 kupitia kipindi cha Asubuhi leo.

Mrida amesema hakuna namna yoyote ya kuwasaidia wafugaji kuepukana na migogoro kama hakuna mpango mkakati wa kuhakikisha wafugaji wanamiliki maeneo yao ya malisho.

Mwenyekiti wa wafugaji taifa ndugu Mrida Mshota, Picha na Adelinus Banenwa

Aidha Mrida amesema kile alichokifanya Mhe Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika ziara yake mkoani Morogoro wilaya ya Mvomero kuwakutanisha mkulima na mfugaji na kupeana mkono wa amani ilikuwa ni ishara inayoonesha dhamira ya dhati ya serikali kutamani migogoro baina ya pande hizo mbili inamalizika.

Sambamba na hilo Mrida amewataka wafugaji kuchangamkia fursa zilizopo hasa suala la umiliki wa mbegu bora za mifugo kama vile Boran na kumiliki mifugo michache ila yenye tija kama ilivyo kwa Afrika ya kusini na Botswana.