Mazingira FM

Mlinzi auawa usiku akiwa  lindoni na watu wanaodhaniwa ni majambazi

23 June 2024, 10:19 pm

Mwanaume mwenye umri wa miaka 72 aliyetambulika kwa jina  la Pastori Mahela mkazi wa Ruselu B kata ya Sazira halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara amekutwa ameuawa usiku

Na Adelinus Banenwa

Mwanaume mwenye umri wa miaka 72 aliyetambulika kwa jina  la Pastori Mahela  mkazi wa Ruselu B kata ya Sazira halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara amekutwa ameuawa usiku wa kuamkia tarehe 23 Juni 2024 katika eneo lake lindo.

Akizungumza na Mazingira Fm mwenyekiti wa mtaa wa Ruselu B Juma Ilega amesema amepokea taarifa za tukio la mlinzi kuuawa majira ya saa 12: 00 asubuhi na alipofika eneo la tukio ni kweli alimkuta mlinzi huyo amelala kifudifudi eneo la tukio huku akionekana kama amepigwa na kitu kichwani ndipo alimpigia diwani simu na jeshi la polisi.

Mwenyekiti  huyo amesema katika eneo la tukio lipo duka moja la nguo ambalo limekutwa limevunjwa na nguo zimeibiwa hivyo anaamini walisababisha kifo cha mlinzi huyo ni majambazi.

Aidha Juma amesema tayari kama  mtaa kwa kushirikiana diwani wa kata ya Sazira na mwenyekiti wa ulinzi shirikishi wamekaa mkutano na wananchi kupanaga mikakati ya kuimarisha ulinzi katika mtaa huo.

Sauti ya mwenyekiti wa mtaa wa Ruselu B Juma Ilega

Michael Kweka diwani wa kata ya Sazira na mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bunda amesema tukio lililotokea ni la kulaani na halikubaliki kwenye jamii na kama viongozi wa kata tayari kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa ya Ruselu A na B wamefanya mkutano na wananchi na wamiliki wa maduka  kuweka mikakati ya kuimarisha usalama katika maeneo hayo.

Mhe Kweka ameongeza kuwa tukio hilo ni la pili katika kipindi cha muda mfupi hivyo ameliomba jeshi la polisi kufanya jitihada za kuwatafuta wahusika wa tukio hilo ili waweze kukamatwa na kuwajibika.

Sauti ya Michael Kweka diwani wa kata ya Sazira

Ryeserwa Rau Mshija mkazi wa Mwakoroba wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambaye ni ndugu wa marehemu amesema tukio hilo kama ndugu wamelipokea kwa masikitiko na wanaliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kubaini nani amehusika na kifo cha ndugu yao.

Mshija amesema aliyefariki ni babu yake na anaitwa Pastori Kija Mahela alizaliwa mwaka 1952 hivyo alikuwa na umri wa miaka 72 na alikuwa na watoto wawili anaowafahamu huku tukio la kuuawa kwake amezipata majira yapata saa mbili asubuhi na alipofika Bunda amekuta tayari mwili wa ndugu yake umeshapelekwa hospitali.

Sauti ya Ryeserwa Rau Mshija ndugu wa marehemu