Bunda Stoo sasa wapata soko lao
21 June 2024, 2:47 pm
“Tumekuwa tukipata tabu sana kutembea umbali mrefu kufuata mboga sokoni hadi manjebe zaidi ya kilometa saba sasa uwepo wa soko hapa ni mkombozi kwetu” wakazi wa Bunda stoo.
Na Adelinus Banenwa
Wakazi wa kata ya Bunda stoo waishukuru serikalai kwa kuwaruhusu kufungua soko katika maeneo yao kwa kuwa ni jambo ambalo walilisubili kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa katika eneo la soko hilo lililopo mtaa wa Idara ya maji kata ya Bunda stoo ambapo wakazi wa kata hiyo walijitokeza kugawiwa maeneo ya kujenga vibanda vya biashara.
Wakizungumza na Mazingira Fm wananchi hao wamesema wamekuwa wakipata changamoto kubwa kwenda mjini kutafuta mahitaji kama vile mboga na mahitaji mengine sokoni, saa nyingine wanalazimika kutumia gharama kubwa kwenda soko kuu kutafuta mahitaji madogo hasa kipindi cha mvua.
Mwenyekiti wa mtaa wa Idara ya maji Mtaki Bwire amesema zoezi lililopo la kuwagawia wananchi maeneo ya kujenga vibanda vya biashara, na wametoa muda hadi miezi sita wawe wamekamilisha .
Amesema uwepo wa soko katika maeneo yao yamejibu kilio cha wananchi wake ambao walikuwa wakilalamika kufuata mahitaji ya nyumbani mbali.
Naye diwani wa kata ya Bunda stoo Flavian Chacha amesema eneo hilo lilitengwa na wananchi tangu mwaka 2014 lakini lilikuwa halijafunguliwa ili wananchi waanze kujenga kwa kuwa serikali ilikuwa haijamaliza kulipa fidia kwa wananchi walio ondolewa hivyo baada ya zoezi la fidia kumalizika tayari ofisi ya mkurugenzi imetoa kibali shughuli za soko kuanza.
Aidha Flavian amesema viongozi wa kata wameweka utaratibu mzuri ambapo kwa yeyote atakayechukua eneo la kujenga kibanda umetolewa muda maalumu wa miezi sita, ikifika na hajajenga basi eneo hilo ananyang’anywa na wanapewa watu wengine walioko tayari.
Pia diwani Flaviani amewashukuru wananchi kwa kujitolea vifaa mbalimbali kujenga choo cha kudumu katika soko hilo ambapo yeye binafsi amechangia trip 2 za mawe kama ishara ya kuwaunga mkono wananchi