Gambi: Marufuku pikipiki hizi kubeba nyara
16 April 2024, 12:13 pm
Viongozi wa CCM ngazi ya kata wakabidhiwa pikipiki waonywa kuzitumia kufanyia uhalifu.
Na Adelinus Banenwa
Wito umetolewa kwa viongozi wa CCM ngazi ya kata waliopata pikipiki za chama kuepuka kutumia vyombo hivyo kufanya uhalifu.
Wito huo umetolewa na Afisa wa kikosi cha usalama barabarani wilaya ya Bunda Inspector Gambi alipohudhuria hafla ya kukabidhi pikipiki kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM ngazi ya kata iliyofanyika viwanja vya ofisi za CCM wilayani Bunda April 12, 2024.
Inspection Gambi amesema ni marufuku pikipiki hizo kukuta zinatumika kubeba nyara za serikali, madawa ya kulevya, samaki waliouawa kwa sumu miongoni mwa uhalifu mwingine.
Gambi amesema anaamini pikipiki hizo zitakwenda kutumika kama matarajio ya chama yanavyotaka na itashangaza sana endapo itafanyika kinyume.
Naye kaimu mkuu wa kikosi cha usalama barabarani wilayani Bunda A/INSP Shaban Mitambo amesema ili kuweka usalama kwa watumiaji wa vyombo hivyo vya moto ni lazima sheria za usalama barabarani kuzingatiwa.
Mitambo amesema ili viongozi hao waweze kutumia pikipiki hizo ni lazima wawe na leseni hiyo ni lazima maana ni takwa kisheria, ni marufuku kubeba abiria zaidi ya mmoja (mshikaki), ni lazima kuvaa kofia ngumu kwa dereva na abiria wake, kuvaa koti na viatu vya kufunika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Bunda Ndugu Mayaya Abraham Magese amesema kiongozi yeyote ambaye pikipiki yake aliyokabidhiwa itakamatwa imebeba magendo au imehusika kufanya uhalifu asijisumbue kumtafuta wala chama hakitahusika na uhalifu huo.