Wananchi watakiwa kupunguza mifugo kulinda mazingira
13 March 2024, 5:48 pm
Mhadhiri wa Chuo cha Kilimo Sokoine SUA Dkt. Lalika amesema kuwa kutokana na uwepo wa mifugo mingi hususani katika eneo la Wegelo unaleta madhara katika bonde la mto Mara hasa uharibifu wa Mazingira.
Na Catherine Msafiri
Katika kutathimini mradi wa dakio la mto Mara mhadhiri wa chuo cha kilimo Sokoine SUA Dkt. Makarius Lalika amewasilisha ripoti ya utafiti unaohusu utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira katika dakio la bonde la mto Mara alioufanya kwa kushirikiana na shirika la uhifadhi wa mazingira WWF Tanzania.
Dkt. Lalika amewasilisha ripoti hiyo 12, March 2024 katika kikao cha WWF na wadau wa mazingira, viongozi wa watumia maji, wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASSA, mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Musoma (MUWASSA) na bodi ya maji bonde la ziwa Victoria.
Akizungumza na radio Mazingira Fm Dkt. Lalika amesema lengo la utafiti huo ni kuangalia namna gani wanufaika wa rasilimali maji wanaweza kuchangia kwenye uhifadhi endelevu wa vyanzo vya maji.
Dkt. Lalika amesema katika utafiti walioufanya waligundua mambo mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu namna ya utekelezaji wa mradi huo.
Sambamba na hayo Dkt. Lalika amebainisha kuwa kutokana na uwepo wa mifugo mingi hususani katika eneo la Wegelo unaleta madhara katika bonde hasa uharibifu wa Mazingira.
Hata hivyo ametoa ushauri kwa wananchi na wafugaji wanaozunguka eneo la bonde kupunguza mifugo ili kuepuka uharibifu wa mazingira.