WWF yatoa msaada wa mizinga ya nyuki kwa jumuiya ya watumiaji maji
12 March 2024, 11:31 am
Shirika la WWF limetoa msaada wa mizinga ya nyuki na miti ya kuotesha kwa jumuiya za watumia maji mkoa wa Mara katika kutunza mazingira ikiwa ni ndani ya mradi wa uhifadhi wa dakio la mto Mara unaosimamiwa na shirika hilo.
Na Catherine Msafiri
Shirika la WWF limetoa msaada wa mizinga ya nyuki na miti ya kuotesha kwa jumuiya za watumia maji mkoa wa Mara katika kutunza mazingira ikiwa ni ndani ya mradi wa uhifadhi wa dakio la mto Mara unaosimamiwa na shirika hilo.
Wakisoma taarifa ya namna walivyotekeleza mradi huo wenyeviti wa jumuiya za watumia maji Tobora juu , Tobora chini na Machira wamesema kwa miezi sita ya mradi wamefanikiwa kubaini maeneo ya vyanzo vya maji , kubaini maeneo ya kuweka mizinga ya nyuki na kufanikisha utunzaji wa vyanzo vya maji kwa kuweka uzio na bikoni.
Taarifa hizo zimesomwa katika mkutano wa WWF walipokuwa wakizungumza na wenyeviti wa watumia maji mkoa wa Mara,maafisa mazingira,Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) pamoja na Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa muembeni compelex Musoma .
Aidha wenyeviti hao wa watumia maji wameishukuru WWF kwa kuwapa ushirikiano pamoja na taasisi ya bonde la ziwa victoria katika kuwapa elimu na vifaa mbalimbali vinavyowasaidia katika kutunza mazingira na vyanzo vya maji.
Hata hivyo shirika la WWF linaratibu Mradi wa Uhifadhi wa Dakio la mto Mara ambao umeanza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika 2025.