WWF, wadau wapima maji mto Tigite-Tarime
26 September 2023, 3:25 pm
Shirika la WWF kwa kushirikiana na bonde la Ziwa Victoria wamefanya zoezi la kupima maji ya mto Tigite uliopo kijiji cha Matongo kata ya Matongo wilaya ya Tarime ili kubaini afya ya mto huo katika vigezo vya asili na vya kisayansi.
Na Thomas Masalu
Shirika la Kuhifadhi Mazingira na Wanyamapori duniani WWF kwa kushirikiana na bonde la Ziwa Victoria wamefanya zoezi la kupima maji ya mto Tigite uliopo kijiji cha Matongo Kata ya Matongo wilaya ya Tarime ili kubaini afya ya mto huo katika vigezo vya asili na vya kisayansi.
Zoezi hilo limefanyika leo 26 Sept, 2023 ambapo limeshirikisha wadau mbalimbali kama vile vikundi vya watumia maji, wapimaji wa afya ya mto ngazi ya jamii, wanafunzi wa shule ya sekondari Matongo na baadhi ya walimu wa shule hiyo.
Zoezi lilianza kwa wadau kupewa elimu katika kutambua umuhimu wa upimaji wa maji ya mto, afya ya mto na vifaa vinayotumika kupimia maji ya mto.
Pamoja na hayo wadau walioneshwa hatua ya kwanza ya upimaji hadi hatua ya mwisho ya upimaji hali iliyoonesha kufurahiwa na wadau kutokana na kupata maarifa mapya katika utuzanji wa vyanzo vya maji.