Serikali yaombwa kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara Bunda
22 September 2023, 5:17 pm
Wafanyabiashara kupitia TCCIA wameiomba serikali kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya kufanya biashara hasa kwa wafanyabiashara waliopanga kwenye majengo ya Umma kama vile stendi na sokoni.
Na Adelinus Banenwa.
Wafanyabiashara kupitia TCCIA wameiomba serikali kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya kufanya biashara hasa kwa wafanyabiashara waliopanga kwenye majengo ya Umma kama vile stendi na sokoni.
Wafanyabiashara wameeleza hayo katika mkutano wa baraza la biashara la wilaya ya Bunda chini ya mwenyekiti ambae ni mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe Dkt. Vicent Anney katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Bunda.
Katika kikao hicho wafanyabiashara waliomba kutafutiwa soko la kudumu la biadhaa na mazao mbalimbali wanayozalisha kama pamba, ngozi, na nyama pia kutoa elimu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa uhakika wa pembejeo za kilimo.
akibainisha changamoto za wakulima wanaopanga kwenye maeneo ya umma mwenyekiti wa wafanyabiashara TCCIA Ndug Magwayega Marwa amesema kuna kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wanaopanga kwenye majengo ya umma ikiwa ni pamoja na uchakavu wa majengo, ulipishwaji wa kodi ya jingo kupitia luku kodi ambayo haiwahusu wao miongoni mwa kero zingine.
Akitolea ufafanuzi katika baadhi ya kero mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa bunda Emmanuel Mkongo amesema suala la uchakavu wa vibanda haliwezi kufanyiwa kazi kwa sasa kupitia fedha za halmashauri kutokana na uwepo wa mradi mkubwa wa ujenzi wa stendi ya kisasa na soko la kisasa.
Mapema watalamu wa Serikali waliwasilisha mbele ya kikao fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Bunda kama vile fursa za Kilimo, Mifugo, Utalii na Biashara, miongoni mwa zingine.
Naye mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Anney amewahakikishia wafanyabiashara kuwa serikali iko pamoja na wao katika kuhakikisha wanafanya biashara zao vizuri bila bugdha huku pia akiwataka wafanyabiashara kutekeleza majukumu yao kama vile kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.