Wilaya ya Bunda yakamilisha kuunda jukwaa wakulima wadogo
22 September 2023, 9:37 am
Imeelezwa kuwa wilaya ya Bunda mkoani Mara, wamekamilisha uundaji wa jukwaa la wakulima wadogo lenye wadau mbalimbali akiwa ni pamoja na wakulima wenyewe.
Na Thomas Masalu
Imeelezwa kuwa wilaya ya Bunda mkoa wa Mara, wamekamilisha uundaji wa jukwaa la wakulima wadogo lenye wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakulima wenyewe.
Jukwaa hilo lina jukumu la kufanya uchechemuzi katika sera za kilimo, sheria, kanuni na miongozo ili kuweza kusaidia mkulima kunufaika na kilimo chake.
Wazo la uundaji wa majukwaa umetokana na mradi wa ASILI-B unaotekekezwa katika halmashauri tano kwa mkoa wa Mara ambapo halmashauri ya mji wa Bunda na halmashauri ya wilaya ya Bunda ni wanufaika wa mradi huo.
Akizungumza na radio Mazingira fm, mratibu wa shirika la BUFADESO, Baraka Kamese ambao pia ndio walezi wa jukwaa hilo amesema kuwa moja ya jukumu kubwa la jukwaa hilo ni kusaidia wadau wa kilimo kukaa na watunga sera au wafanya maamuzi kwa ngazi ya halmashauri na idara nyingine katika kutatua changamoto za wakulima wadogo.