Mtanda atoa maagizo kwa viongozi wa Serengeti na Tarime
13 September 2023, 4:35 pm
Viongozi wa Wilaya ya Serengeti na Tarime wasimamie sheria zilizowekwa ili kulinda vyanzo vya maji ya Mto Mara
Na Edward Lucas
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda amewaagiza viongozi wa Wilaya ya Serengeti na Tarime kukaa pamoja na kusimamia sheria ndogondogo katika ulinzi wa vyanzo vya maji katika bonde la Mto Mara.
Mtanda ametoa kauli hiyo leo 13 Sept 2023 wakati wa zoezi la upandaji wa miche na uwekaji wa bikoni au vigingi katika eneo la kijiji cha Borenga Wilaya ya Serengeti ikiwa ni katika hatua ya kuadhimisha siku ya Mto Mara.
Maagizo hayo ya Mhe. Mtanda yamekuja kufuatia malalamiko aliyoyapokea kutoka kwa wananchi na viongozi wa maeneo hayo kuhusu changamoto wanayokumbana nayo kuhusu Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika bonde la Mto Mara
Ambapo akizungumzia hali hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma amesema kumekuwa na mgogoro katika eneo hilo baina ya wakazi wa Serengeti na Tarime kuhusu jambo linalopelekea kukosekana usimamizi mzuri wa vyanzo vya maji
Awali akisoma taarifa ya risala ya utekelezaji wa zoezi la upandaji wa miti na uwekaji wa bikoni kando ya Mto Mara, Afisa Mazingira Halmashauri ya Wilaya Serengeti, Helga Enock Nkongoki imeeleza mikakati inayoendelea ili kulinda na kuhifadhi vyanzo vya mto Mara