Serengeti: Kifo cha kusikitisha mtoto aliyetelekezwa nje ya nyumba ya babu yake
23 August 2023, 12:03 am
Mtoto wa mwaka mmoja na miezi 6 Ismail Erasto amefariki dunia katika kifo cha kuhuzunisha na kusikitisha baada ya bodaboda kwenda kumtelekeza nje nyumbani kwa babu yake kijiji cha Mabuli wilaya ya Serengeti
Na Edward Lucas
Tukio la kusikitisha na kuhuzunisha mtoto wa mwaka mmoja na miezi 6 Ismail Erasto Benjamini amefariki dunia ikiwa ni siku mbili tangu taarifa ya kutelekezwa kwa babu yake kijiji cha Mabuli kata ya Nyambureti wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Katika tukio hilo inaelezwa kuwa siku ya Alhamisi tarehe 17 Agosti 2023 majira ya saa 12:00 asubuhi mtoto huyo akiwa na dada yake walipelekwa nyumbani hapo na mwendesha pikipiki yaani bodaboda ikielezwa ameagizwa na shangazi wa watoto hao kisha kuwaacha na kuondoka.
Akizungumza na Mazingira Fm Jeremia Benjamini ambaye ni baba mkubwa wa watoto hao amesema wakiwa wamelala walisikia muungurumo wa pikipiki ikifika nyumbani kwao na walipotoka walimkuta bodaboda anawashusha watoto hao ambapo mmoja kati yao (Ismail ambaye ni marehemu kwa sasa) alionekana hali yake sio nzuri na baada ya kumuuliza alisema ameagizwa na shangazi yao aitwaye Norah awalete hapo nyumbani kisha yeye akaondoka.
Katika hatua nyingine Mazingira fm ilimtafuta shangazi wa watoto hao Norah Benjamini ambaye amekiri kuwasafirisha kwa bodaboda kutoka Buhemba wilaya ya Butiama alipokuwa akiishi nao hadi kijiji cha Mabuli kwa babu yao huku akitaja sababu ya kufanya hivyo ni kutokana na kuelemewa na hali ya maisha hususani katika kumhudumia Ismail ambaye alikuwa anaugua mara kwa mara na wazazi wa mtoto huyo kutompatia ushirikiano.
Aidha Mazingira FM iliwatafuta wazazi wa watoto hao (Erasto Benjamini na Neema Lugendo) ambao walionesha kurushiana lawama ya jukumu la malezi ya watoto huku ikibainika kuwa hata kutengana kwao moja ya sababu ni mtoto huyo Ismail ambapo baba anatuhumu kuwa mtoto sio wake mwanamke huyo alizaa na mtu mwingine.
Kufuatia hali hiyo uongozi wa kijiji cha Mabuli umeielekeza familia kukaa na kujadili kisha kupeleka taarifa katika uongozi wa kijiji ukieleza ni kwa namna gani hao watoto wengine wawili waliobakia watalelewa