Wakazi Bunda Stoo walia ukosefu wa maji
18 August 2023, 10:18 am
Suala la maji katika Mtaa wa idara ya maji hasa maeneo ya panda miti imekuwa ni kikwazo ambapo wamesema hulazimika kuamka usiku wa manane ili kwenda kufata maji.
Na Adelinus Banenwa
Wakazi Mtaa wa Idara ya Maji kata ya Bunda Stoo Halmashauri ya Mji wa Bunda wamelalamikia ukosefu wa maji licha ya mabomba makubwa ya kusambaza maji yanapitia katika eneo lao.
Wakizungumza katika kikao kilichoitishwa na Mhe Diwani wa kata hiyo Flavian Chacha wakazi hao wamesema suala la maji katika Mtaa wa Idara ya Maji hasa maeneo ya Panda Miti imekuwa ni kikwazo ambapo wamesema hulazimika kuamka usiku wa manane ili kwenda kufata maji.
Aidha wamebainisha kuwa wanalazimika kuchimba mashimo ili kupata maji ambayo kawaidi maji hayo si safi na salama kwa matumizi ya binadamu
Akijibu kiro hiyo diwani wa kata hiyo Mhe Flavian amesema serikali kupitia mamlaka ya Maji Bunda inaenda kutekeleza mpango wa kutandaza mabomba ya maji katika maeneo ya Panda miti na maeneo mengine ya kata ya Bunda stoo
Mhe Flavian amesema kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi inasema inakwenda kumtua mama ndoo kichwani hivyo lazima itekelezwe.
Mbali na suala la maji pia diwani huyo alielezea mipango mingine ya serikali katika kata hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara, shule mpya ya msingi inayogharimu shilingi mil 540, ujenzi hospitali mpya ya Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa shilingi bil 1.5 miongoni mwa miradi mingine.
Aidha Mhe Flavian amewataka wananchi kujenga tabia ya kuhudhuria mikutano inayoitishwa na Viongozi ili waweze kupata majibu ya maswali yao badala ya kwenda kuzungumzia mtaani.