Mikakati kupambana na wanyama waharibifu yawekwa wazi Bunda
21 July 2023, 9:12 pm
Kuongeza magari, kuweka uzio wa waya na kuongeza vituo vya vikosi vya kudhibiti wanyamapori waharibifu ni miongoni mwa mikakati iliyojadiliwa katika kusaidia kilio cha wananchi wanaopakana na hifadhi ya Serengeti jimbo la Bunda.
Na Edward Lucas
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dr. Vicent Naano ameahidi kusimamia upatikanaji wa magari mawili ili kusaidia juhudi za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Dr Naano amebainisha hayo kupitia mkutano ulioratibiwa na mbunge wa jimbo la Bunda mheshimiwa Boniphace Mwita Getere ukiwakutanisha wananchi, viongozi na taasisi za uhifadhi pamoja na wadau wa uhifadhi ili kujadili mikakati ya kukabiliana na wanyama hao.
Akizungumzia mkakati huo, Kamishna Msaidizi TAWA, Said Kabanda amesema jambo la kukabiliana na wanyamapori waharibifu linahitaji ushirikiano wa wadau wote wakiwemo wananchi na taasisi zingine ili kufanikisha zoezi
Kwa upande wake Mbunge Boniphace Getere amezitaka mamlaka na taasisi husika kuangalia uwezekano wa kuweka uzio wa waya kama wananchi walivyoomba.