Matumaini ya kupanda bei ya pamba yazidi kufifia kwa wakulima Simiyu
9 July 2023, 10:53 pm
Tangu kufunguliwa msimu wa pamba mwezi Mei 2023 bei haijaongezeka hata senti moja kutoka bei elekezi iliyotangazwa na serikali shilingi 1,060 kwa kilo moja.
Na Edward Lucas
Matumaini ya wakulima juu ya ushindani wa bei kwa kampuni za ununuzi wa pamba mkoa wa Simiyu yanazidi kufifia ikiwa ni takribani miezi miwili tangu kuzinduliwa kwa msimu lakini bado bei ni shilingi 1,060 kwa kilo.
Hilo limebainika kupitia mahojiano ya Mazingira Fm na baadhi ya viongozi wa vituo vya ununuzi wa pamba Julai 9, 2023 ilipotembelea katika vituo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kijiji cha Lutubiga, Mkula na Sapiwi kwa lengo la kujionea zoezi la ununuzi wa pamba linavyoendelea.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema licha ya kuwepo kampuni nyingi katika ununuzi wa pamba hadi sasa hakuna hata kampuni moja iliyoongeza hata senti moja kutoka katika bei elekezi ya shilingi 1,060.
Viongozi hao wamesema jambo pekee la ushindani katika vituo vyao limesalia katika dhana ya ubora wa mizani ambapo wakulima hukimbilia katika vituo ambavyo wanaamini mzani una ubora zaidi na iwapo kituo cha ununuzi wa pamba kina fedha za kumlipa mkulima kwa wakati.
Bei ya pamba kwa msimu uliopita mwaka 2022 iliuzwa hadi shilingi 2,200 licha ya bei elekezi kuwa shilingi 1,560 kwa kilo moja.