CHADEMA: Ugumu wa maisha kwa vijana chanzo cha kucheza kamari, kubeti
21 June 2023, 10:40 am
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimefanya mkutano katika kata ya Bunda Stoo halmashauri ya mji wa Bunda huku wakigusia mambo mbalimbali likiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana na ugumu wa maisha.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya kata hadi taifa akiwemo mwenyekiti wa baraza la vijana Chadema taifa John Pambalu, katibu mkuu wa vijana taifa Yohana Kaunya miongoni mwa viongozi wengine
Akizungumza katika mkutano huo Yohana Kaunya ambaye alikuwa mgombea udiwani kata ya Bunda Stoo katika uchaguzi mkuu 2020 na katibu mkuu CHADEMA Taifa amesema amekuja kuwashukuru wakazi wa kata ya Bunda Stoo kwa kura walizompa pia amesema ukosefu wa ajira bado ni changamoto ili hali vijana wasomi wapo.
Aidha katibu huyo wa vijana amesema amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa kata ya Bunda Stoo kuhusu mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na bili ya maji kuwa juu, ubovu wa miundombinu ya barabara, changamoto ya watu TASAF miongoni mwa changamoto zingine.
Naye mwenyekiti wa BAVICHA John Pambalu amesema kuwa tatizo la ugumu wa maisha bado ni kubwa sana katika taifa pia ukosefu wa ajira kwa vijana kunasababisha vijana wengi kushindwa kufanya kazi badala yake wanakwenda kwenye michezo ya kubahatisha.
Aidha amesema baraza la vijana Chadema litaadhimisha siku ya vijana duniani mkoani Mbeya ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 12 Augosti ambapo amewataka vijana kukutana ili kujua mustakabali wao.