Kamati ya siasa CCM Bunda imeielekeza serikali wilayani Bunda kutatua changamoto katika shule za msingi ikiwemo upungufu wa madawati.
19 January 2023, 7:08 am
Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Bunda ikiongozwa na mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bunda Ndugu Ibrahim Magesse Mayaya imefanya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya Cha hicho ndani ya Jimbo la Bunda Mjini.
Ziara hii imefanyika katika miradi ya elimu, Afya, barabara maji na umeme ambapo zimetembelewa kata za Kabarimu, Sazira, Kabasa, Wariku, Guta, Bunda stoo na Nyamakoko.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni shule za msingi Kabarimu A na B kata ya Kabarimu mradi wa Maji Bitaraguru, mradi wa kituo Cha Afya Wariku, Mradi wa Chujio la Maji Nyabehu lililoghalimu Bilioni Kumi, hospital ya Halmashauri ya Mji wa Bunda pamoja na shule ya Sekondari Nyamakokoto.
Katika ziara hii Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bunda Ndugu Ibrahim Magesse Mayaya amesema serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi imeleta fedha nyingi kwa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo hivyo ni wajibu wa wasimamizi kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa vizuri.
Aidha changamoto zilizoainishwa katika ziara hiyo ni pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa, madawati na matundu ya vyoo katika shule za msingi, upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari, upungufu wa watumishi idara ya Afya katika zahanati ya sazira miongoni mwa changamoto zingine Kamati ya siasa kupitia kwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bunda Ndugu Mayaya imeitaka serikali kuhakikisha changamoto zilizoainishwa kwenye sekta ya elimu kufanyiwa Kazi ikiwemo upungufu wa madawati jambo linalopelekea watoto kukaa Chini.