Mpanda FM

Mpanda yazindua kampeni ya usafi kudhibiti taka

19 October 2026, 10:36 am

Vifaa vilivyotolewa kwaajili ya kuhifadhia taka mtaani. Picha na Friday Mwangomale

“tunahitaji kuondoa changamoto ya kurundika na kutupa taka hovyo ili mji wetu uwe safi“

Na. Friday Mwangomale

Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph, amekabidhi vifaa vya kutunzia taka na mabango kwa watendaji wa Kata na Mitaa kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kudumisha utamaduni wa kufanya usafi kwa wananchi wa Manispaa ya Mpanda.

Dc Jamila amekabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni ishirini Oktoba 17, 2026 katika uzinduzi wa kampeni ya usafi iliyoratibiwa na mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Mpanda, Bi. Sigilinda Mdemu, nakuzinduliwa katika eneo la Stendi ya Zamani, Kata ya Kashaulili manispaa ya Mpanda.

Katika zoezi hilo mkuu wa wilaya amewataka wananchi wa manispaa ya Mpanda kuhakikisha kuwa wanakuwa na utamaduni wa kuhifadhi taka kwenye vyombo maalumu vya kutunzia taka badala ya kuzitupa hovyo, hali inayoweza kuchochea uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha afya zao.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Mpanda

Aidha Jamila pia amewakumbusha wananchi kuendelea kuzingatia na kuchukua hatua madhubuti kuhusiana na mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni, kama inavyoelekezwa na mamlaka za hali ya hewa.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bi. Sigilinda Mdemu, ameahidi kuendelea kusimamia zoezi la usafi katika maeneo ya manispaa kwa kushirikisha askari mgambo katika kutekeleza zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kutoza faini kwa watakaokiuka taratibu za usafi kwa kutupa taka hovyo ili kuhakikisha mji wa Mpanda unakuwa safi na mazingira yanaboreshwa.

Vifaa vilivyotolewa katika zoezi hilo la usafi ni pamoja na mabango ya tahadhari na onyo kuhusu athari za kutupa taka hovyo na Mapipa maalumu ya kuhifadhia taka, ambayo yamesambazwa kwenye maeneo yote stendi za magari na masoko.